Judges 8:3-23

3 aMungu amewatia Orebu na Zeebu, hao viongozi wa Wamidiani, mikononi mwenu. Je, mimi niliweza kufanya nini kulinganisha na mlichofanya ninyi?” Aliposema hili, hasira yao dhidi yake ikatulia.

4 bGideoni akiwa pamoja na wale watu 300 waliofuatana naye, wakiwa wamechoka na wenye njaa lakini bado wakiwafuatia, wakafika Yordani na kuuvuka. 5 cAkawaambia watu wa Sukothi, “Tafadhali lipatieni jeshi langu mikate, kwa maana wamechoka, nami ningali ninawafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani.”

6 dLakini maafisa wa Sukothi wakasema, “Je, mikono ya Zeba na Salmuna tayari mnayo sasa ili tuweze kulipatia jeshi lako mikate?”

7Gideoni akajibu, “Kwa ajili ya hilo tu, Bwana atakapowatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, nitaichana nyama ya miili yenu kwenye miiba ya nyikani na kwenye michongoma.”

8 eKutoka hapo alikwea mpaka Penieli na kutoa ombi lile lile, lakini nao watu wa Penieli wakamjibu kama watu wa Sukothi walivyokuwa wamemjibu. 9Hivyo akawaambia watu wa Penieli, “Nitakaporudi baada ya kushinda, nitaubomoa mnara huu.”

10 fWakati huu Zeba na Salmuna walikuwa Karkori wakiwa na jeshi lenye watu wapatao 15,000 wale wote waliokuwa wamesalia wa mataifa ya mashariki, kwa kuwa watu wapatao 120,000 wenye panga walikuwa wameuawa. 11 gBasi Gideoni akakwea kwa njia ya wasafiri mashariki ya Noba na Yogbeha na kulishambulia jeshi ambalo halikushuku lolote. 12Zeba na Salmuna, hao wafalme wawili wa Midiani, wakakimbia lakini yeye Gideoni akawafuata na kuwakamata, akalishinda hilo jeshi lao lote.

13 hGideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani kwa kupitia Mwinuko wa Heresi. 14 iAkamkamata kijana mmoja wa Sukothi na kumuuliza maswali, naye yule kijana akamwandikia majina ya maafisa sabini wa Sukothi, ambao ni viongozi wa mji. 15Ndipo Gideoni akaja na kuwaambia watu wa Sukothi, “Tazama, hapa wapo Zeba na Salmuna mlionisimanga kwa ajili yao mkisema, ‘Je, mikono ya Zeba na Salmuna tayari mnayo sasa ili tuweze kulipatia jeshi lako mikate?’ ” 16 jAkawachukua hao viongozi wa mji na kuwafundisha watu wa Sukothi somo kwa kuwaadhibu kwa miiba na michongoma ya nyikani. 17Pia akaubomoa mnara wa Penieli na kuwaua watu wa mji.

18 kKisha akawauliza Zeba na Salmuna, “Ni watu wa aina gani mliowaua huko Tabori?”

Wakajibu, “Ni watu kama wewe, kila mmoja wao akiwa na nafasi ya uana wa mfalme.”

19 lGideoni akajibu, “Hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu hasa. Hakika kama aishivyo Bwana, kama mngekuwa mmewaacha hai, mimi nisingewaua ninyi.” 20Akamgeukia Yetheri, mwanawe mzaliwa wa kwanza, akasema, “Waue hawa!” Lakini Yetheri hakuufuta upanga wake, kwa sababu aliogopa, kwa kuwa alikuwa bado kijana mdogo tu.

21 mZeba na Salmuna wakasema, “Njoo ufanye hivyo wewe mwenyewe. ‘Alivyo mtu, ndivyo zilivyo nguvu zake.’ ” Hivyo Gideoni akatoka mbele na kuwaua, naye akayaondoa mapambo kwenye shingo za ngamia zao.

Kisibau Cha Gideoni

22Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Ututawale, wewe, wanao na wana wa wana wako, kwa kuwa umetuokoa kutoka mikononi mwa Wamidiani.”

23 nLakini Gideoni akawaambia, “Mimi sitatawala juu yenu, wala wanangu hawatatawala juu yenu. Bwana ndiye atakayetawala juu yenu ninyi.”
Copyright information for SwhNEN